MAPENZI
Mapenzi ni kitu kilichowekwa na Mungu ndani ya kila
mwanadamu. Mapenzi ni kitu kilicholala na huamka yenyewe kwa wakati ambao Mungu
amepanga kwa kila mtu. Hivyo mapenzi yapo ndani ya kila mtu tangu anapozaliwa,
ila huwa yamelala, na yana muda wake wa kuamka.
“Nawasihi enyi binti za
Yerusalemu,… msiyachochee mapenzi wala kuyaamsha, hata yatakapoona vema
yenyewe”
(Wimbo 2 :7)
Utakubaliana nami kuwa huwezi kuamsha
kitu ambacho hakijalala, kwa hiyo mapenzi huwa yamelala. Anaposema ‘yatakapoona
vema yenyewe’ maana yake Mungu alikwisha yapangia utaratibu na muda wake ili
yaamke. Kumbuka kila kitu alichokifanya Mungu ni kizuri na chema hivyo alijua hali
halisi ya ujana, hali yetu ya kibayolojia ndiyo maana akaweka muda wa mapenzi
kuamka. Biblia inasema mapenzi huweza kuamshwa na mtu mwenyewe.
![]() |
| Ni wale tu wenye kwenda na muda na majira ufikia ndoto zao |
“…enyi binti za Yerusalemu,…msiyachochee mapenzi wa
la kuyaamsha…”
(Wimbo 2 :7)
Maana yake wewe mwenyewe unao uwezo wa kuyachochea na
kuyaamsha. Inawezekana ukafikiri ni sawa au ni vema tu kuyachochea na kuyaamsha
mapenzi wakati wowote, lakini jiulize kwa nini Mungu aliyawekea utaratibu (guarantee)
ya muda maalumu wa kuamka ? Sikiliza, Mungu amevipa vitu vyote kufanywa kwa
muda aliyepanga yeye kwa sababu vitu hivyo huwa vizuri vinapofanyika kwa muda
huo. Ooh ! Haleluya ! Unapofanya kitu chochote hata kama ni kizuri ukikifanya
kwa muda usio wa Mungu kitu au jambo hilo linakuwa si jema tena linakuwa
dhambi, na haliwi lenye faida.
”Kwa kila jambo kuna
majira yake na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu, …je mtendaji anayo faida
gani katika yale anayojishughulisha nayo ? Nimeona taabu ambayo Mungu amewapa
wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati
wake, ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya
tangu mwanzo hata mwisho”
(Muhubiri 3 :1,9-11)
Lazima ujue kuwa Mungu alikwishaandaa mpango na utaratibu
mzuri wa maisha yako tangu enzi.
“Kumbuka mambo ya zamani
za kale maana mimi ni Mungu wala hapana aliye kama mimi, nitangazaye mwisho
tangu mwanzo na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado, nikisema shauri
langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote”
(Isaya 46 :10)
Mungu anaposema nitangazaye mwisho tangu mwanzo, maana yake
aliufahamu mwanzo wako hata mwisho wako. Alijua utazaliwa lini, utazaliwa wapi
na nani na alijua utaoa au utaolewa lini na nani na utaishi wapi. Na katika
yote hayo Mungu anakuwazia mawazo mema na mpango wake juu maisha yako ni mwema.
Ni lazima uelewe hili, Mungu anaposema, shauri langu litasimama maana yake
anategemea yote aliyokupangia, ukikubali na kutii yote akuagizayo, hataacha
kutimiza yote aliyokupangia ambayo ni mema (maana hakukupangia jambo baya),
mazuri na mwisho wake ni uzima wa milele.
Sikiliza mpendwa, Mungu humaliza kwanza halafu ndipo anaanza.
Ooh ! Haleluya ! Maana yake ni hii yeye aliratibu maisha yako na kukupangia
matukio yote hata mwisho, akaona ni vema ndipo akaruhusu uwepo duniani. Tatizo
kubwa ni watu kutojua na kutotaka kujua kalenda ya Mungu kwao na hivyo hutafuta
njia za mkato (shortcut ) na ndipo uangamivu huja juu yao.
“Maana ninajua mawazo
ninayowawazia nnyi asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa
ninyi tumiani siku zenu za mwisho”
(Yer 29 :11)
Kukuwazia amani, maana yake ni kuwa
na maisha mazuri ya furaha hapa duniani. Na anaposema ‘kuwapa ninyi tumaini la
siku zenu za mwisho’ uwe na uhakika ni uzima wa milele. Hivyo hata utaratibu wa
mapenzi upo ndani ya mpango wa Mungu. Watu wengi husumbuka kutafuta utaratibu
wao badala ya kumwachia Mungu awaongoze katika utaratibu ulio mzuri na ulio
bora.
Vijana wengi hushindwa kuishi
sawasawa na mpango wa Mungu aliowapangia, na wengi wao si kwa sababu hawataki
ila ni kwa sababu hawaijui siri hii kubwa ambayo Mungu ameiweka ndani yao.
Unauliza siri ipi, soma Muh 3 :11 Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake,
tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao ,… Ni vema uitambue siri hii
itakusaidia.
Kwa hiyo mapenzi yamewekewa muda wake
wa kuamka, kwa hiyo ukiyaamsha kwa muda wako unaotaka wewe, unakuwa umejitoa
katika utaratibu au mpango wa Mungu na kuiendea njia yako binafsi, ambayo
mwisho wake ni dharau ya milele yaani Jehanamu. Mara nyingi baada ya vijana
kutoka katika mpango wa Mungu na kukutana matatizo makubwa na mazito katika
maisha yao hujaribu kuyatatua kwa kutumia akilia zao. Na mara nyingi hufanya
maamuzi yasiyo sahihi na hivyo hupata matatizo makubwa zaidi na kusahau
kumtegemea Yesu aliye mshauri wa ajabu na mfalme wa amani.
Sikiliza, Uhusiano wowote ni lazima
uanzishwe na Yesu mwenyewe ili uhusiano uwe bora, unaompa Mungu utukufu na
wenye faida katika maisha yako. Biblia inaeleza jambo hili wazi kabisa, Muh 3
:9 Je mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo ? Ahaa !
Kumbe hakuna faida bali ni hasara tupu kujishughulisha upendavyo wewe na sio
kama apendavyo Mungu.
![]() |
| Je unazani huu ni muda na wakati sahihi wa kuyaamsha mapenzi? |
Ndugu mpendwa, hupaswi kuyachochea
wala kuyaamsha mapenzi. Inawezekana unatenda matendo au unazungumza maneno
ambayo hufanya mapenzi ya wengine kuamka, maana yake umeyachochea, na hii ni
chukizo kwa Bwana. Pengine hufanyi ngono lakini umekuwa ukiwafanya wengine
waendelee kufanya hivyo. Maana yake ni kwamba unatumiwa na Shetani kama wakala
(Agent) wake. Inawezekana unajiuliza utayachocheaje mapenzi ya wengine kuamka ?
Tembea yako, tazama yako, uvaaji wako, maneno yako na matendo yako yanaweza
kabisa kuchochea mapenzi ya wengine kuamka. Ooh, hilo ni somo jingine, Mungu
akipenda tutajifunza.
MAANA YA GIRLFRIEND NA BOYFRIEND
Kwanza tuangalie maana halisi ya kawaida ya girlfriend na
boyfriend, halafu tuangalie maana halisi anayoitumia Shetani, ambayo imefunikwa
kwa maneno mazuri yaani girlfriend na boyfriend, kama mtu awekavyo chakula
kizuri katika mtego wa panya.
Neno friend lina maana rafiki, girl
ni msichana na boy ni mvulana. Sasa ukiyaunganisha maneno hayo, unapata rafiki
wa kike au rafiki wa kiume. Hii ni maana ya kawaida ya girlfriend na boyfriend,
si mbaya kwa jinsi unvyoyasikia maneno hayo. Kumbuka Shetani hutumia maneno
mazuri akiwa na maana au kusudi la kwake tofauti ambalo ni chukizo kwa Mungu.
Na huwateka watu wasipofahamu undani halisi na wasio na macho ya kiroho yaani
ufahamu wa rohoni wa kutambua mbinu za Ibilisi. Jambo kubwa hapa si kuvijua
vitu au kuyaelewa maneno yanayotajwa, ila ni kufahamu maana halisi ya hayo
unayoyasikia katika ufahamu wa rohoni. Haleluya! Ndiyo maana ipo karama ya
kupambanua roho.
Mpendwa ni vema uwe makini sana na
kila unalolifanya. Wapo watu wanaotetea uovu wakidai wana ufahamu wa roho au
wamefunuliwa na roho. Sikiliza, kuwa na roho au kufunuliwa mambo fulani na roho
si tatizo, ila tatizo ni roho ya namna gani uliyonayo au ni roho wa nani
aliyekufunulia unayotuambia.
“Wapendwa msiiamini kila roho bali
zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo
wengi wametokea duniani.”
(1 Yohana 4:1)
Mara nyingi Shetani hutumia maneno
mazuri, kumbuka alivyomjaribu Yesu. Mathayo 4:6 "Akamwambia, ukiwa ndiwe mwana
wa Mungu jitupe chini, kwa maana imeandikwa atakuagizia malaika zake; na
mikononi mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe". Haya ni
maneno mazuri na pia ni kweli yameandikwa, soma Zaburi 91:11-12 "Kwa kuwa
atakuagizia malaika zake... mikononi mwao watakuchukua; usije ukajikwaa mguu
wako katika jiwe". Lakini ulikuwa ni mtego wa kumtaka Yesu awe na kiburi ili
ajikweze au ajitukuze kuwa yeye ndiye mwana wa Mungu. Bwana Yesu aliitambua
maana halisi au maana ya ndani iliyifichika, kwa kupambwa kwa maneno mazuri
aliyoyataja Shetani, na ndiyo maana Yesu alishinda. Kushinda kwa Yesu si kwa
sababu ya kuyaelewa maneno ya Shetani bali ni kufahamu maana ya maneno yale kwa
tafsiri ya rohoni. Kwa hiyo huwezi kuona ubaya wa kuwa na girlfriend au
boyfriend usipokuwa na ufahamu wa rohoni ambao ndiyo unaotuwezesha kutambua
maana halisi zilizofichika.
Hebu jiulize mwenyewe; Unaposema girlfriend au boyfriend
wangu ndani yako, moyoni mwako huwa unajisikiaje, unapata hisia gani na huwa
unafikiri nini hasa akilini mwako unapotamka hivyo?
*********ITAENDELEA SEHEMU YA NNE (4)*********



No comments:
Post a Comment