UTANGULIZI
"Mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa injili ya Kristo"
(Wafilipi 1:27)
Na ashukuriwe Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, yeye aliyeniwezesha kuandika somo hili. Somo hili litakuwezesha na kukusaidia kuelewa undani wa Girlfriend na Boyfriend na kuona njia ipasayo ya uzima. Vijana wengi siku hizi huambiana nakupenda lakini hawajui nini maana halisi ya UPENDO au huambiana hivyo kiunafiki tu. Ni vema ufahamu utaratibu wa mapenzi jinsi ulivyopangwa na Mungu katika maisha yako. Maana huo utaratibu umewekwa ndani ya moyo wako tangu enzi, na wengi hawafahamu jambo hili.
“Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake tena ameifanya hiyo milele ndani ya mioyo yao , ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya tangu mwanzo hata mwisho."
(Muhubiri 3:11)
KWA NINI MUNGU AMEUMBA TOFAUTI ZA JINSIA?
Tendo la kujamiiana au tendo la ndoa limewekwa na Mungu mwenyewe kwa makusudi maalum na kwa utaratibu mzuri kabisa. Mungu
hakuweka tofauti za jinsia kwa mwanadamu peke yake, bali pamoja na viumbe wengine. Lakini pana tofauti kubwa ya makusudi halisi ya kuweka tofauti kwa mwanadamu na kuweka tofauti hizo kwa viumbe wengine.
hakuweka tofauti za jinsia kwa mwanadamu peke yake, bali pamoja na viumbe wengine. Lakini pana tofauti kubwa ya makusudi halisi ya kuweka tofauti kwa mwanadamu na kuweka tofauti hizo kwa viumbe wengine.
“Mungu akasema maji nayajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu… na kila ndege arukaye kwa jinsi yake. …Mungu akasema nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake… na wanyama wa mwituni kwa jinsi zake ikawa hivyo”
(Mwanzo 1:20-25)
Mungu anaposema kwa jinsi zake maana yake viumbe vyenye jinsia na namna tofauti. Aliumba namna hizo tofauti kwa NENO tu, lakini mwanadamu aliumbwa kwa neno (na tumfanye mtu kwa mfano wetu…) na kwa vitendo. Maana Mungu alimfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi na akamfanya mwanamke kwa kutumia ubavu wa mwanamume. Uumbaji wa mwanadamu ni tofauti sana na viumbe wengine.
Viumbe wengine wote waliumbwa kwa jinsia na namna tofauti kwa ajili ya kuendeleza uumbaji (recreation) na pia kwa matumizi ya mwanadamu. Mojawapo ya sababu za kuumbwa kwa mwanamke na mwanamume ni;
-Kuendeleza uumbaji wa Mungu
-Kuvitawala vitu vyote
-Kuitiisha nchi
-Kusaidiana
“Bwana Mungu akasema si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi a kufanana naye”
(Mwanzo 2:18)
Wanyama hawakuambiwa hivi.
Mungu anapofanya kitu huwa na kusudi na utaratibu maalum wa alichokifanya. Tendo la ndoa liliwekwa na Mungu kwa makusudi maalum na aliweka utaratibu wake na malengo maalaum. Tendo la ndoa limekuwa chanzo cha matatizo mengi makubwa kwa mwanadamu si kwa sababu tendo la ndoa ni baya, ila ni kwa sababu watu wanalifanya nje ya wakati wa Mungu, na wanalifanya isivyotakiwa yaani kinyume na utaratibu na makusudi ya Mungu. Wengi huwa hawajui ya kuwa tendo la ndoa linatakiwa kufanywa kwa utukufu wa Mungu. Kwa mwanadamu tendo la ndoa huwaunganisha watu wawili wa jinsia tofauti kuwa mwili mmoja na huambatana na furaha ya hisia za ndani ambazo hukamilishwa kwa UPENDO. Ndiyo maana wavulana wengi wanapokuwa wakitongoza husema NAKUPENDA, ila siku hizi hata wasichana hutongoza. Hii ni kwa sababu upendo hukamilisha ndoa. Ndoa ni moja ya jambo ambalo Mungu amempa mwanadamu ili limpatie mwanadamu furaha na kamwe sio kwa ajili ya huzuni, hasira au matatizo. Lakini siku hizi ndoa imekuwa kama mwiba; maana watu wengi hudhani ndoa ni kama sehemu ya starehe na hawaichukulii ndoa kama sehemu ya kumtukuza Mungu.
Upendo chanzo chake halisi ni Mungu mwenyewe. Tangu enzo ya uumbaji Mungu alimpenda mwanadamu, na ndiyo maana mwanadamu alipoasi Mungu hakumwangamiza mara, bali alimwokoa na kuurejesha upendo halisi kwa njia ya Yesu Kristo. Katika Biblia Yesu ni Bwana arusi na kanisa ni Bibi arusi, na ndiyo maana kuna upendo wa ajabu wa Yesu kwa kanisa.
UPENDO NI NINI?
Mara nyingi vijana hudanganyana kwa kuambiana nakupenda lakini hawajui nini maana halisi ya upendo au wakati mwingine wanakuwa na upendo wa kinafiki. Upendo ni hali ya ndani ya moyo au nafsi na huelezwa kwa maneno na kwa matendo makuu mazuri yafanywayo kutoka ndani ya moyo. Upendo hauangalii gharama za kufanya tendo la upendo. Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe pekee ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele”
Kiasi cha upendo uliokuwamo ndani ya Mungu kwa mwanadamu, ndiyo uliomfanya Mungu kuwa tayari kumtoa mwanawe, tena wa pekee, maana yake hakuwa na mwingine lakini alimtoa kwa ajili ya uzima wetu. Kiasi cha upendo uliokuwamo ndani ya moyo wa Ibrahimu, alivyompenda Mungu ndiyo uliomfanya Ibrahimu kuwa tayari kumtolea Mungu mwamawe Isaka awe sadaka ya kuteketezwa, japo alikuwa ni mwana pekee tena aliyempata uzeeni. Si jambo rahisi lakini upendo hauhesabu gharama iliyopo katika kutenda. Maana upendo huambatana na imani ndani ya mtu. 1 Korintho 13:4-8 “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu, hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wowote;…”
Kiasi cha upendo uliokuwamo ndani ya Yesu kwa mwanadamu, ulimfanya Yesu kuwa tayari kuutoa uhai wake, akafa msalabani kwa ajili yetu. Sasa mpendwa msomaji unaweza ukaelewa nini maana ya halisi upendo. Wenzetu husema ‘To love is a very great responsibility’ Siku hizi watu wengi hutumia neno nakupenda ili kukidhi haja ya tamaa zao, hawana upendo ila ni unafiki mtupu umejaa ndani mwao. Pendo lisiwe na unafiki….
SHETANI HUTUMIA MANENO MAZURI
Mara nyingi Shetani hutumia maneno mazuri, aidha yameanzishwa na Mungu au ya kibiblia ili apate kuwapoteza watu wengi. Na vijana wengi hawajui jambo hili na hivyo wengi wao hujikuta mikononi mwa Shetani na hawajui cha kufanya na mwishowe huangamizwa kabisa. Tazama mifano ifuatayo;
· Neno mpenzi lina maana nzuri ki-Biblia, 1 Kor 7:1 “Basi wapenzi wangu kwa kuwa tuna ahadi hizo na tujitakase” Maana yake anawapenda mno. Rumi 9:25 “…nitawaita watu wangu wale wasio watu wangu, na mpenzi wangu yeye asiye mpenzi wangu”
Mpenzi ni mtu yule umpendaye sana na sio upendo wa kinafiki. Si rahisi kutambua ukweli wa maneno unayoambiwa na mtu, ni lazima uwe na macho ya rohoni na ufahamu wa rohoni. Maana Roho wa Mungu ndiye ajuaye mambo yaliyo ndani ya moyo wa mtu. Wapo vijana wengi ambao huambiana ‘naomba uwe mpenzi wangu’ ila ndani yao hawana nia nzuri’ Sasa wewe utajuaje kuwa huyo anayekutaka uwe mpenzi wake ana nia mbaya na wewe na ametumia neno zuri, mpenzi au nakupenda? Roho Mtakatifu anahitajika.
Girlfriend na Boyfriend ni maneno mazuri kabisa, huyatumia kwa maana ya kwake na kuwafanya vijana waingie kwenye mtego wake bila kujua. Ni lazima umuelewe Shetani na mbinu zake ndipo utakapoweza kumshinda kwa kutumia neno la Mungu. Maana Shetani hujigeuza, unashangaa!! Soma 2 Kor 11:14 “Wala si ajabu, maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru”
Tunapotega samaki huwa tunaweka chakula chao kwenye ndoana ili wavutiwe na hatimaye wananaswa na ndoana. Vilevile katika kutega ndege au panya ni lazima uweke chakula kidoga, ambacho kitawavutia na hivyo huweza kunaswa na mtego kirahisi. Sasa na Shetani naye huweka vitu vizuri katika mambo mbalimbali kuwavutia vijana na wengi wao hunaswa na mtego kwa kuona vitu vizuri badala ya kuona mtego, maana macho yao ya rohoni hayaoni yametiwa giza . Na mara nyingi huwa hawana neno la kutosha ndani yao na hivyo hutumia akili zao kujaribu kupambanua kila kitu. Mpendwa naomba ujiulize, hivi kwa akili yako binasi bila msaada wa Mungu unaweza kujua na kutambua kuwa anayekuomba uwe mpenzi wake hakudanganyi au hana pendo la kinafiki?
JE NI VEMA KUWA NA GIRLFRIEND AU BOYFRIEND?
Vijana wengi hujiuliza swali hili. Na wengi wao huona kuwa ni vema tena yafaa, lakini hawajui maana halisi ya girlfriend na boyfriend na wala hawajui zilianzaje. Kama nilivyokueleza hapo mwanzo, Shetani hutumia maneno mazuri akiwa na maana ya kwake tofauti tena mbaya ili awateke watu. Kabla ya kulijibu swali hili na kueleza maana ya girlfriend na boyfriend na chanzo chake kibiblia ni vema ufahamu undani juu ya mapenzi na jinsi Mungu alivyoweka utaratibu wa mapenzi katika maisha ya kila mtu.
MAPENZI
Mapenzi ni kitu kilichowekwa na Mungu ndani ya kila mwanadamu. Mapenzi ni kitu kilicholala na huamka yenyewe kwa wakati ambao Mungu amepanga kwa kila mtu. Hivyo mapenzi yapo ndani ya kila mtu tangu anapozaliwa, ila huwa yamelala, na yana muda wake wa kuamka.
“Nawasihi enyi binti za Yerusalemu,… msiyachochee mapenzi wala kuyaamsha, hata yatakapoona vema yenyewe”
(Wimbo 2 :7)
Utakubaliana nami kuwa huwezi kuamsha kitu ambacho hakijalala, kwa hiyo mapenzi huwa yamelala. Anaposema ‘yatakapoona vema yenyewe’ maana yake Mungu alikwisha yapangia utaratibu na muda wake ili yaamke. Kumbuka kila kitu alichokifanya Mungu ni kizuri na chema hivyo alijua hali halisi ya ujana, hali yetu ya kibayolojia ndiyo maana akaweka muda wa mapenzi kuamka. Biblia inasema mapenzi huweza kuamshwa na mtu mwenyewe. Wimbo 2 :7 “…enyi binti za Yerusalemu,…msiyachochee mapenzi wala kuyaamsha…” Maana yake wewe mwenyewe unao uwezo wa kuyachochea na kuyaamsha. Inawezekana ukafikiri ni sawa au ni vema tu kuyachochea na kuyaamsha mapenzi wakati wowote, lakini jiulize kwa nini Mungu aliyawekea utaratibu (gerentee) ya muda maalumu wa kuamka ? Sikiliza, Mungu amevipa vitu vyote kufanywa kwa muda aliyepanga yeye kwa sababu vitu hivyo huwa vizuri vinapofanyika kwa muda huo. Ooh ! Haleluya ! Unapofanya kitu chochote hata kama ni kizuri ukikifanya kwa muda usio wa Mungu kitu au jambo hilo linakuwa si jema tena linakuwa dhambi, na haliwi lenye faida. Muhubiri 3 :1,9-11 Kwa kila jambo kuna majira yake na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu, …je mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo ? Nimeona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake, ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya tangu mwanzo hata mwisho"
Lazima ujue kuwa Mungu alikwishaandaa mpango na utaratibu mzuri wa maisha yako tangu enzi. Isaya 46 :10 “Kumbuka mambo ya zamani za kale maana mimi ni Mungu wala hapana aliye kama mimi, nitangazaye mwisho tangu mwanzo na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado, nikisema shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote” Mungu anaposema nitangazaye mwisho tangu mwanzo, maana yake aliufahamu mwanzo wako hata mwisho wako. Alijua utazaliwa lini, utazaliwa wapi na nani na alijua utaoa au utaolewa lini na nani na utaishi wapi. Na katika yote hayo Mungu anakuwazia mawazo mema na mpango wake juu maisha yako ni mwema. Ni lazima uelewe hili, Mungu anaposema, shauri langu litasimama maana yake anategemea yote aliyokupangia, ukikubali na kutii yote akuagizayo, hataacha kutimiza yote aliyokupangia ambayo ni mema (maana hakukupangia jambo baya), mazuri na mwisho wake ni uzima wa milele.
Sikiliza mpendwa, Mungu humaliza kwanza halafu ndipo anaanza. Ooh ! Haleluya ! Maana yake ni hii yeye aliratibu maisha yako na kukupangia matukio yote hata mwisho, akaona ni vema ndipo akaruhusu uwepo duniani. Tatizo kubwa ni watu kutojua na kutotaka kujua kalenda ya Mungu kwao na hivyo hutafuta njia za mkato (shortcut ) na ndipo uangamivu huja juu yao. Yer 29 :11 Maana ninajua mawazo ninayowawazia nnyi asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumiani siku zenu za mwisho »
Kukuwazia amani, maana yake ni kuwa na maisha mazuri ya furaha hapa duniani. Na anaposema ‘kuwapa ninyi tumaini la siku zenu za mwisho’ uwe na uhakika ni uzima wa milele. Hivyo hata utaratibu wa mapenzi upo ndani ya mpango wa Mungu. Watu wengi husumbuka kutafuta utaratibu wao badala ya kumwachia Mungu awaongoze katika utaratibu ulio mzuri na ulio bora.
Vijana wengi hushindwa kuishi sawasawa na mpango wa Mungu aliowapangia, na wengi wao si kwa sababu hawataki ila ni kwa sababu hawaijui siri hii kubwa ambayo Mungu ameiweka ndani yao. Unauliza siri ipi, soma Muh 3 :11 Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake, tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao ,… Ni vema uitambue siri hii itakusaidia.
Kwa hiyo mapenzi yamewekewa muda wake wa kuamka, kwa hiyo ukiyaamsha kwa muda wako unaotaka wewe, unakuwa umejitoa katika utaratibu au mpango wa Mungu na kuiendea njia yako binafsi, ambayo mwisho wake ni dharau ya milele yaani Jehanamu. Mara nyingi baada ya vijana kutoka katika mpango wa Mungu na kukutana matatizo makubwa na mazito katika maisha yao hujaribu kuyatatua kwa kutumia akilia zao. Na mara nyingi hufanya maamuzi yasiyo sahihi na hivyo hupata matatizo makubwa zaidi na kusahau kumtegemea Yesu aliye mshauri wa ajabu na mfalme wa amani.
Sikiliza, Uhusiano wowote ni lazima uanzishwe na Yesu mwenyewe ili uhusiano uwe bora, unaompa Mungu utukufu na wenye faida katika maisha yako. Biblia inaeleza jambo hili wazi kabisa, Muh 3 :9 Je mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo ? Ahaa ! Kumbe hakuna faida bali ni hasara tupu kujishughulisha upendavyo wewe na sio kama apendavyo Mungu.
Ndugu mpendwa, hupaswi kuyachochea wala kuyaamsha mapenzi. Inawezekana unatenda matendo au unazungumza maneno ambayo hufanya mapenzi ya wengine kuamka, maana yake umeyachochea, na hii ni chukizo kwa Bwana. Pengine hufanyi ngono lakini umekuwa ukiwafanya wengine waendelee kufanya hivyo. Maana yake ni kwamba unatumiwa na Shetani kama ajenti wake. Inawezekana unajiuliza utayachocheaje mapenzi ya wengine kuamka ? Tembea yako, tazama yako, uvaaji wako, maneno yako na matendo yako yanaweza kabisa kuchochea mapenzi ya wengine kuamka. Ooh, hilo ni somo jingine, Mungu akipenda tutajifunza.
MAANA YA GIRLFRIEND NA BOYFRIEND
Kwanza tuangalie maana halisi ya kawaida ya girlfriend na boyfriend, halafu tuangalie maana halisi anayoitumia Shetani, ambayo imefunikwa kwa maneno mazuri yaani girlfriend na boyfriend, kama mtu awekavyo chakula kizuri katika mtego wa panya.
Neno friend lina maana rafiki, girl ni msichana na boy ni mvulana. Sasa ukiyaunganisha maneno hayo, unapata rafiki wa kike au rafiki wa kiume. Hii ni maana ya kawaida ya girlfriend na boyfriend, si mbaya kwa jinsi unvyoyasikia maneno hayo. Kumbuka Shetani hutumia maneno mazuri akiwa na maana au kusudi la kwake tofauti ambalo ni chukizo kwa Mungu. Na huwateka watu wasipofahamu undani halisi na wasio na macho ya kiroho yaani ufahamu wa rohoni wa kutambua mbinu za Ibilisi. Jambo kubwa hapa si kuvijua vitu au kuyaelewa maneno yanayotajwa, ila ni kufahamu maana halisi ya hayo unayoyasikia katika ufahamu wa rohoni. Haleluya! Ndiyo maana ipo karama ya kupambanua roho.
![]() |
| U Boyfriend na U Girlfriend ndiyo unaleta uasherati ndani ya kanisa. |
Mpendwa ni vema uwe makini sana na kila unalolifanya. Wapo watu wanaotetea uovu wakidai wana ufahamu wa roho au wamefunuliwa na roho. Sikiliza, kuwa na roho au kufunuliwa mambo fulani na roho si tatizo, ila tatizo ni roho ya namna gani uliyonayo au ni roho wa nani aliyekufunulia unayotuambia. 1 Yohana 4:1 Wapendwa msiiamini kila roho bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.
Mara nyingi Shetani hutumia maneno mazuri, kumbuka alivyomjaribu Yesu. Mathayo 4:6 Akamwambia, ukiwa ndiwe mwana wa Mungu jitupe chini, kwa maana imeandikwa atakuagizia malaika zake; na mikononi mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Haya ni maneno mazuri na pia ni kweli yameandikwa, soma Zaburi 91:11-12 Kwa kuwa atakuagizia malaika zake... mikononi mwao watakuchukua; usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Lakini ulikuwa ni mtego wa kumtaka Yesu awe na kiburi ili ajikweze au ajitukuze kuwa yeye ndiye mwana wa Mungu. Bwana Yesu aliitambua maana halisi au maana ya ndani iliyifichika, kwa kupambwa kwa maneno mazuri aliyoyataja Shetani, na ndiyo maana Yesu alishinda. Kushinda kwa Yesu si kwa sababu ya kuyaelewa maneno ya Shetani bali ni kufahamu maana ya maneno yale kwa tafsiri ya rohoni. Kwa hiyo huwezi kuona ubaya wa kuwa na girlfriend au boyfriend usipokuwa na ufahamu wa rohoni ambao ndiyo unaotuwezesha kutambua maana halisi zilizofichika.
Hebu jiulize mwenyewe; Unaposema girlfriend au boyfriend wangu ndani yako, moyoni mwako huwa unajisikiaje, unapata hisia gani na huwa unafikiri nini hasa akilini mwako unapotamka hivyo?
....................................................ITAENDELEA SEHEMU YA PILI............................................

No comments:
Post a Comment